Jumapili , 29th Jan , 2023

Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) leo January 29,2023 limetangaza matokeo ya mitihani ya kidato cha nne mwaka 2022 ambapo Watahiniwa wa Shule 456,975 kati ya Watahiniwa 520,558 wenye matokeo ambao ni sawa na 87.79% wamefaulu kwa kupata madaraja kuanzia daraja la kwanza, hadi la nne

“Kati yao Wasichana 243,285 (87.08%) na Wavulana ni 213,690 (88.60%), ufaulu huu wa Watahiniwa wa Shule umeongezeka kwa 0.49% ikilinganishwa na mwaka 2021”

Aidha Baraza la Mitihani (NECTA) limefuta matokeo yote ya Watahiniwa wanne wa kidato cha nne mwaka 2022 walioandika lugha za matusi katika mitihani yao.

Baraza la Mitihani pia limeyafuta matokeo yote ya Watahiniwa 333, mmoja wa QT na 332 wa Mtihani wa kidato cha nne ambao wamebainika kuwa wamefanya udanganyifu kwenye mtihani

"Matokeo hayo yamefutwa kwa mujibu wa kifungu cha 5 (2) (I na J) cha Sheria ya Baraza la Mitihani sura ya 107 kikisomwa pamoja na kifungu cha 30 (2) (b) cha kanuni za mtihani mwaka 2016"

Baraza la mitihani NECTA limesitisha utaratibu wa kutangaza shule bora na mwanafunzi bora wa matokeo ya kidato cha nne

Kaimu katibu Mtendaji wa Baraza la mitihani Tanzania NECTA Athumani Salumu Amasi amesema utaratibu huo wa kutangaza shule bora ulikuwa unazitangazia biashara baadhi ya shule

"Kutangaza shule ya kwanza huenda tulikuwa tunakufanyia Marketing kwa kuitaja tu hiyo shule, shule zipo nyingi zaidi ya elfu 18, sasa unapotaja moja sidhani kama ina tija" amesema Athumani Salumu 

Kuhusu kumtangaza mwanafunzi bora wa mtihani huo amesema hakuna tija katika hilo kwani hauwezi kumtangaza mwanafunzi mmoja katika ya wanafunzi wote Tanzania ambao huenda pia mazingira yao ya kusoma yalikuwa tofauti

"Unamtaja mtu kwamba ameongoza katika kundi ambalo pamoja na kwamba wamefanya mtihani huo huo lakini hawakusoma katika mazingira yanayofanana, alafu sasa unampa sifa mtu mmoja" amesema Athumani Salumu