Jumapili , 26th Dec , 2021

Askofu wa Afrika Kusini na Mshindi wa tuzo ya Nobel Desmond Tutu, ambaye aliisaidia Afrika Kusini kumaliza ubaguzi wa rangi amefariki dunia leo Desemba 26, 2021 Cape Town, akiwa na umri wa miaka 90.

Askofu Desmond Tutu

Kifo cha Desmond Tutu kimetangazwa na Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini ambaye amesema kwamba kifo cha mtumishi huyo wa kanisa kimeadhimisha kwa mara nyengine misiba ya kizazi muhimu cha taifa hilo.

Alishiriki katika vita dhidi ya ubaguzi wa rangi akishirikiana na Nelson Mandela, na kuchochea harakati za kukomesha sera ya ubaguzi wa rangi iliyotekelezwa na serikali ya wazungu wachache dhidi ya weusi walio wengi nchini Afrika Kusini kuanzia 1948 hadi 1991.

Alitunukiwa tuzo ya Nobel mwaka 1984 kwa jukumu lake katika mapambano ya kukomesha mfumo wa ubaguzi wa rangi.

Askofu Desmond Tutu akiwa na Nelson Mandela enzi za uhao wao.

Kifo cha Tutu kinajiri wiki chache tu baada ya Rais wa mwisho wa enzi za ubaguzi wa rangi FW de Clerk , kufariki akiwa na umri wa miaka 85.

Historia yake katika utumishi wa kanisa

Askofu Desmond Tutu, alitawazwa kama Padri mwaka wa 1960, na kuhudumu kama askofu wa Lesotho kuanzia 1976-78, askofu msaidizi wa Johannesburg na mkuu wa Parokia ya Soweto.

Alikuwa Askofu wa Johannesburg mnamo 1985, na akateuliwa kuwa Askofu Mkuu wa kwanza mweusi wa Cape Town. 

Alitumia nafasi yake ya hadhi ya juu kuzungumzia ukandamizaji dhidi ya watu weusi nchini mwake, siku zote akisema nia yake ni ya kidini na si ya kisiasa.