Ijumaa , 20th Mei , 2022

Mwanamume mmoja nchini Kenya Jacob Ochola ameibuka na kudai mgao wa mali za aliyekuwa Rais wa tatu wa Kenya Mwai Kibaki akieleza kuwa yeye ni mtoto wa kwanza wa Kibaki.

Jacob Ochola

Ochola anadai kuwa akiwa na miaka 21 alifahamishwa kuwa Kibaki ni baba yake na wakaanza kuwa na mahusiano mazuri

Anasema mama yake aliolewa akiwa mtoto mdogo na ndio maana jina lake la ukoo linatoka katika jamii ya Wajaluo. 

Katika mahojiano na chombo kimoja cha habari nchini Kenya Ochola anasema baada ya kifo cha baba yake mlezi, ndipo mama yake alimfahamisha kuwa marehemu si baba yake mzazi.

"Nilizaliwa Julai 22, 1960, Kaloleni, Nairobi. Nilikua nikijua mimi ni Mluo. Nilikuja kujua kwamba sikuwa Mjaluo nilipofikisha miaka 21. Mwaka mmoja baada ya mtu niliyemfahamu kuwa ni baba yangu kufariki, mama yangu alinieleza kuwa aliyefariki si baba yangu mzazi, aliniambia pia anaenda kuongea na baba yangu kwa sababu anataka kuniona alifanya hivyo baada ya mwezi mmoja hivi. Huu ndio wakati nilipata fursa ya kukutana na rais wa zamani," amenukuliwa Ochola 

Aidha ameeleza kuwa wakati Mwai Kibaki akiwa hai alikuwa akimtembelea mara kadhaa kwa siri katika hoteli moja nchini Kenya na kuonana naye

Hakuna taarifa yoyote iliyotolewa na upande wa familia ya Rais huyo wa zamani wa Kenya kuhusu mtu huyo 

Vyanzo vya habari nchini Kenya vinadai mali za kiongozi huyo zina  thamani ya KSh150 bilioni ambapo mwanaume huyo anasema anahitaji kujumuishwa katika mgao wa mali hizo