Alhamisi , 30th Mar , 2017

Bajeti ya Kenya ya mwaka 2017/2018, imesomwa leo kinyume na inavyosomwa kawaida mwezi Juni, kutokana na uchaguzi mkuu utakaofanyika Agosti mwaka huu, huku ikitangaza kusimamisha ajira katika sekta ya umma.

Waziri wa Fedha wa Kenya, Henry Rotich

Katika bajeti hiyo ya shilingi za Kenya trilioni 2.6 (Takriban shilingi trilioni 52 za Tanzania) Waziri wa Fedha, wa nchi hiyo, Henry Rotich ameondoa kodi kwenye mahindi yanayoagizwa kutoka nje kwa kipindi cha miezi minne ijayo,

Kuondoa kodi kwenye mahindi ni hatua ambayo inaweza kukufanya uiite bajeti hiyo kuwa ni 'bajeti ya ugali' kutokana kutokana na chakula kinachotumia rasilimali hiyo ya mahindi kuwa ni ugali.

Aidha kodi imeondolewa kwenye dawa za kuulia wadudu za nchini humo pamoja na magari ya utalii yanayoundwa nchini Kenya.

Katika bajeti hiyo ambayo ni ya mwisho kwa serikali ya Jubilee katika muhula wake wa kwanza, serikali imeongezea kodi kwenye kamari hadi 50% kutoka 7.5% ya awali kama njia ya kukomesha uchezaji kamari.

Serikali pia imetangaza kusimamisha ajira katika sekta za umma isipokuwa sekta ya elimu kama njia ya kupunguza matumizi.

Jumla ya Shilingi bilioni 524.6 za kenya katika bajeti hiyo zitatokana na mikopo kutoka nje na ndani ya nchi.

Shilingi bilioni 2 zimetengwa kuwaajiri walimu, na zingine bilioni 4 kuwalipia mtihani wanafunzi wa darasa la nane na kidato cha nnemwaka 2017 na 2018 huku serikali za kaunti zikipata jumla la shilingi bilioni 329.

Ili kuhakikisha kuwa vijana wana ajira, serikali imetenga shilingi milioni 450 kwa kuboresha kiwanda cha Rivatex, na zingine milioni 250 kuboresha kiwanda cha maziwa cha New KCC.

 

NB: Fedha ziliztajwa ni shilingi za Kenya