Jumamosi , 22nd Oct , 2022

Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, David Concar amesema kuwa maofisa waandamizi wa Jeshi la Polisi wanapaswa kuwa makini na uwasilishwaji wa taarifa kwa umma ili kuepuka baadhi ya watu wengine kuzibadilisha taarifa kwa lengo la kupotosha wananchi wakati wa majanga na dharura.

Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, David Concar.

Balozi David Concar amesema hayo leo Oktoba 22, 2022, wakati akifunga mafunzo awamu ya pili ya kuwajengea uwezo wa mawasiliano maafisa wa jeshi hilo wakati wa majanga na dharura yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Kwa upande wake Kamishina wa Intelijensia ya Makosa ya Jinai CP Charles Mkumbo, amewataka washiriki kutumia mafunzo hayo vizuri ambapo yatawajengea uwezo mkubwa wa kutoa taarifa zinazozingatia vigezo ili kuepuka kutoa taarifa za upotoshaji katika jamii.
  
Aidha Jessie Beham, mmoja wa wawezeshaji wa mafunzo hayo kutoka taasisi ya Global Communications Academy ya nchini Uingereza, amesema mafunzo hayo ni muhimu kwa maofisa wa polisi na maofisa wa serikali kwa ujumla ambapo amebainisha kuwa yatawajengea uwezo katika kufanya mawasiliano wakati wa dharura na majanga pindi yanapotokea.

Naye Dkt. Richard Sambaiga, mmoja wa wawezeshaji wa mafunzo hayo kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, amesema mafunzo hayo yatawajengea uwezo kwa kutambua msingi na sayansi katika mawasiliano na namna ya kukabiliana na majanga nchini.