Jumatano , 2nd Jan , 2019

Serikali ya Somalia imemwamuru balozi wa Umoja wa Mataifa nchini humo, Nicholas Haysom kuondoka baada ya kumtuhumu kuwa ameingilia masuala ya ndani ya taifa hilo.

Nicholas Haysom.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje wa nchi hiyo imesema Haysom hatokaribishwa tena Somalia na hawezi kuendelea kuendesha shughuli zake nchini humo.

Haysom alikosoa kukamatwa na kuuawa kwa waandamanaji waliokuwa wakilalamikia kukamatwa kwa kiongozi wa zamani wa Al-Shabab, Sheikh Mukhtar Robow Abu Mansurmjini Baidoa kati ya Desemba 13 na 15 mwaka uliopita.

Haysom alimwandikia barua Waziri wa Mambo ya Ndani wa Somalia, Mohamed Abukar Islow na kuzungumzia uzito wa taarifa ambazo zilikuwa zimewahusisha wanajeshi wanaoungwa mkono na UN na kukamatwa kwa kiongozi huyo.

Barua ya Hayson ilikuwa na maswali mengi kuhusu hatua zilizochukuliwa na serikali wakati wa makabiliano yaliyotokea Baidoa, jimbo la Kusini Magharibi wakati wa kumakatwa kwa naibu kiongozi wa zamani wa Al-Shabab mwezi uliopita.