Jumatatu , 18th Mar , 2024

Serikali ya awamu ya sita kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) inaendelea na jitihada za kuhakikisha kuwa miundombinu ya barabara na madaraja mkoani Ruvuma inaimarishwa ili kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji wa watu na bidhaa mbalimbali kwa ajili ya kuinua Uchumi.

Barabara ya Songea – Makambako km 295

Katika kipindi cha miaka mitatu ya Uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Serikali imeendelea na utekelezaji wa Miradi ya mikubwa ya Ujenzi wa Barabara, Madaraja na na Viwanja vya ndege, ikiwa ni pamoja na barabara ya Mbinga – Mbamba bay km 66 ambayo imekamilika na Ujenzi wa Daraja la Ruhuhu lenye urefu wa mita 98.01 ambalo linaunganisha Wilaya za Nyasa Mkoani Ruvuma na Wilaya ya Ludewa Mkoani Njombe.

Akizungumza na Waandishi wa Habari tarehe 14 Machi 2024; Meneja wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma Mha. Salehe Juma Mkwama amesema vile vile Serikali imefanya Ukarabati na Ujenzi wa Kiwanja cha Ndege Songea na inaendelea na Ujenzi wa kiwango cha lami katika Barabara ya Kitai -Lituhi - Ndumbi km 95. 3; inayoelekea Bandari ya Ndumbi, ambayo pia inatumika kusafirisha Makaa ya Mawe.

Amesema kutokana na kutumika muda mrefu na hivyo kuchakaa; Serikali ipo mbioni kujenga upya barabara ya Songea – Makambako km 295 na imekusudia kujenga Daraja la Mitomoni, Barabara ya Likuyufusi hadi Mkenda km 124 ikijumuisha ujenzi wa Daraja la Mkenda linalounganisha nchi ya Tanzania na Msumbiji katika mto Ruvuma na Ujenzi wa Barabara ya Lupiro – Malinyi – Kilosa kwa Mpepo – Londo – Kitanda – Lumecha km 512 ambayo inaunganisha mikoa ya Ruvuma na Morogoro.

Mha. Salehe amesema pia Serikali kupitia TANROADS imefanya usanifu katika Barabara za Mbamba bay – Lituhi km 112.4, barabara ya Mtwarapachani – Nalasi – Tunduru km 300, Barabara ya Unyoni – Maguu – Kipapa km 25, Barabara ya Nangombo – Chiwindi km 40, na Barabara ya Madaba – Mundindi (Liganga) – Mkiu km 35.

Ameongeza kuwa TANROADS Mkoa wa Ruvuma inasimamia mizani 4 kwa ajili ya kudhibiti magari yasizidishe uzito na kuharibu barabara, ambazo zipo katika vijiji vya Lipokela kwenye barabara ya Songea – Mbinga, Luhimba kwenye barabara ya Songea – Lukumburu, Sisi kwa sisi kwenye barabara ya Tunduru – Lumesule na Kijiji cha Buruma katika barabara ya Mbinga – Mbamba Bay.