Jumanne , 4th Mei , 2021

Baraza la Wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, BAWACHA limekanusha madai ya kuwa chama chao kina mfumo dume, kwa kusema kuwa chama hicho ndicho chama pekee chenye wajumbe wengi wanawake.

Mjumbe Kamati Kuu Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, Suzan Kiwanga

Akizungumza leo na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam, Mjumbe Kamati Kuu CHADEMA, Suzan Kiwanga, mara baada ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai kuagiza Katibu Mkuu CHADEMA kuandika barua ambayo ataambatanisha na katiba ya chama na muhtasari wa kikao kilichofanya maamuzi ya kuwafukuza uanachama wabunge 19 wa chama hicho, amesema BAWACHA watashughulikia suala la wabunge hao kwa mujibu wa katiba.

“Chama chetu hakina mfumo dume kama ambavyo inasambazwa huko, sisi ndio chama pekee chenyewe wajumbe wengi wanawake Kamati Kuu kuliko chama chochote cha Siasa Tanzania, Chama chetu ndio kilikuwa na wagombea wengi wanawake majimboni, ambapo tulikuwa zaidi ya 60 majimboni tofauti na chama chochote” amesema  Suzan Kiwanga

Wakiongelea suala la wabunge 19 na yale yaliyobainishwa na Spika Ndugai BAWACHA wameeleza kushangazwa na mkinzano uliopo katika ofisi ya spika kutokana na kutofautiana kwa taarifa, huku wakiendele kusema kuwa CHADEMA haiwatambui wabunge hao.

“Wakati Spika anawaondoa Bungeni waliokuwa Wabunge wa CUF Bunge lililopita Spika hakuomba hivyo vielelezo anavyoviomba kwetu, ametukosea sana kuita barua yetu kipeperushi, Hao anaowaita Wabunge sisi hatuwatambui tunawaona wasaliti tu katika Chama, tuliwaita kwenye kikao cha Kamati Kuu tuwasikilize lakini hawakutokea” amesema  Suzan Kiwanga