Alhamisi , 26th Mar , 2026

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio linalotambua kuwa biashara ya utumwa dhidi ya Waafrika kuwa ni uhalifu mbaya zaidi dhidi ya ubinadamu.

Azimio hilo lililopendekezwa na Ghana lilitaka biashara haramu ya utumwa wa kuvuka bahari ya Atlantiki kutambuliwa kama uhalifu mbaya zaidi katika historia ya binadamu licha ya upinzani mkali kutoka Ulaya na Marekani.

Pia Umoja wa Mataifa umezitaka nchi zilizohusika kulipa fidia kama hatua thabiti katika kurekebisha makosa ya kihistoria.

Baraza hilo lenye wanachama 193 lilipitisha azimio hilo kwa kura 123 za ndio, kura 3 za kupinga ambazo ni za Argentina, Israel na Marekani huku nchi 52 zikijizuia. 

Uingereza na nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya walikuwa miongoni mwa wale waliojizuia.

Azimio hilo pia linahimiza kurejeshwa haraka na bila vikwazo katika nchi za asili kwa vitu vyote vya kitamaduni, ikiwa ni pamoja na kazi za sanaa, vifaa vya makumbusho, hati na kumbukumbu za kitaifa.