''Bora mzee wa ubwabwa kuliko wetu'' - Maalim Seif

Jumanne , 20th Oct , 2020

Mgombea urais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo Taifa, Maalim Seif Sharif Hamad amesema kuwa amesikitishwa na suala la mgombea urais wa Tanzania kupitia chama hicho, Bernard Membe kusema ataendelea kuwania urais kinyume na msimamo wa chama.

Maalim Seif na Bernard Membe

Maalim Seif ametoa kauli hiyo leo Oktoba 20, 2020 Jijini Dar es Salaam, wakati akiongea na vyombo vya habari, ambapo amesema kuwa msimamo wa kumuunga mkono mgombea urais wa CHADEMA Tundu Lissu, ulitolewa na chama cha ACT-Wazalendo na wala sio wa kiongozi mmoja mmoja.

Maalim Seif ameeleza kuwa wao kama ACT-Wazalendo waliamua hivyo baada ya kuona mgombea urais wao haonekani kwenye kampeni kama wagombea wengine wa vyama vingine na wakaamua wamuunge mkono Tundu Lissu kutoka CHADEMA.

“Tuliona mgombea urais wetu haonekani kwenye kampeni za uchaguzi mkuu, bora hata Mzee wa ubwabwa kuliko mgombea wetu, ndio maana tukakubaliana kumuunga mkono Lissu,” - alisema Maalim Seif.

Maalim Seif ameongeza kuwa, “ACT- Wazalendo tulimwambia mapema Bernard Membe, wakati anakuja kwenye chama chetu, kwamba katika hiki kitu cha uchaguzi huwa tunashirikiana na chama makini na alikubali”.