Ijumaa , 25th Dec , 2015

Iringa mjini hali si shwari ndani ya Chama cha Mapinduzi ambapo tangu kumalizika kwa mchakato wa uchaguzi huo kumekuwa na shutuma na kutuhumiana kwa wazi wazi baina ya viongozi wa chama hicho.

Mwenyekiti wa CCM, mkoa wa Iringa Bibi. Jescar Msambatavangu

Katika kile kinachothibitisha kuwepo mtafaruku ndani ya chama hicho ngazi ya mkoa baadhi ya viongozi wa chama hicho wamekuwa wakimtuhumu mwenyekiti wa CCM, mkoa wa Iringa Bibi. Jescar Msambatavangu kukisaliti chama hicho na kusaidia upinzani hali iliyosababisha chama hicho kupooza vibaya kwenye uchaguzi huo huku mwenyekiti huyo naye akishusha tuhuma kwa baadhi ya viongozi kutumia kundi la vijana kumzushia tuhuma mbalimbali.

Wakati mwenyekiti huyo wa chama akishusha tuhuma hizo upande wa pili wa wanaomsakama kusaliti chama chake akiwemo Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho mkoa wa Iringa Dkt. Yahaya Msigwa anasema adhabu ya usaliti kwenye chama hicho kwa mujibu wa kanuni ni kufukuzwa uanachama.

Wakati haya yakiendelea Kaimu Katibu wa CCM, mkoa wa Iringa Elisha Mwampashi amesema ni vyema chama kikafanya uchunguzi wa kina na kujiridhisha kabla ya kumchukulia hatua mtu yeyote kwani uamuzi wowote usio wa hekima unaweza kukiumiza chama badala ya kutatua changamoto kwa njia zilizo salama.

katika uchaguzi mkuu wa Oktoba ngazi ya ubunge na udiwani jimbo la Iringa mjini mgombea wa CCM, Fredrick Mwakalebela alishindwa na mgombea wa ubunge wa chama cha CHADEMA, Mchungaji Peter Msigwa huku pia chama hicho kikipoteza kata 14 kati ya 18 za jimbo hilo na hivyo kushindwa kupata kiti cha meya kuongoza halmashauri ya manispaa ya Iringa hali ambayo imeacha sintofahamu ndani ya chama hicho.