Jumamosi , 29th Aug , 2020

Chama cha Mapinduzi (CCM), leo kimezindua kampeni zake za mbio za Urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28 mwaka huu na kuhudhuriwa na wananchi wengi pamoja na wasanii mbalimbali nchini huku mgombea wake Dkt Magufuli akiahidi kwa wananchi.

Rais Dkt John Pombe Magufuli

Uzinduzi wa kampeni hizo umefanyika hii leo katika Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma, ambapo Rais Magufuli amewataka Watanzania kuwasikiliza wagombea wote kwenye kampeni zao ili waweze kujua ni nani wataweza kumchagua.

"Tumeanza kipindi cha kampeni watakuja wengi na mtaelezwa mengi, wito wangu kwenu wasikilizeni kwa makini ili siku ya kupiga kura mfanye maamuzi sahihi, uchaguzi huu utaamua pia tupate viongozi wa aina gani, wa kuteletea maendeleo au tupate viongozi wenye ajenda zao binafsi", amesema Rais Magufuli.

Aidha Rais Magufuli ameeleza sababu iliyopelekea yeye kumchagua tena Mama Samia Suluhu kuwa mgombea mwenza, "Ndiyo maana niliamua tena kumchagua Mama Samia Suluhu kuwa mgombea mwenza, sikutaka kuchagua mwingine wa kuja kujifunza, pia ni mzuri mnamuona mwenyewe alivyo mweupe ni mchapakazi na anajua kutekeleza malengo ya Watanzania bila kubagua vyama vyao".