Jumamosi , 27th Jun , 2015

Wanachama watano wa chama cha Demokrasia na maendeleo (CHADEMA) jimbo la Dodoma Mjini wamejitokeza kuwania kiti cha ubunge katika jimbo hilo akiwemo mkurugenzi wa oganaizesheni na mafunzo, Benson Kigaila.

Benson Kigaila

Dodoma. Wanachama watano wa chama cha Demokrasia na maendeleo (CHADEMA) jimbo la Dodoma Mjini wamejitokeza kuwania kiti cha ubunge katika jimbo hilo akiwemo mkurugenzi wa oganaizesheni na mafunzo, Benson Kigaila.

Akizungumza na East Africa Radio ofisini kwake mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Dodoma, Bwn Mambo Jella , amesema kuwa miongoni mwa wanachama hao wapo wapo wafanyabiashara na wajasiriamali mbalimbali.

Amewataja wanachama wengine waliorudisha fomu zao jana ambayo ndiyo ilikuwa ni siku ya mwisho kwa wawania ubunge na udiwani wa chama hicho kurudisha fomu zao kuwa ni pamoja na Said Kitegile, Filbert Mhoja ambaye ni mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (BAVICHA) Wilaya ya Dodoma mjini, Emmanuel Nollo na Josephina Kihoza ambaye ni mwenyekiti wa asasi za kiraia ambaye amechukua fomu ya jimbo pamoja na fomu ya viti maalum.

Kwa upande wa ubunge viti maalum ni Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa (CHADEMA (BAWACHA) mkoa wa Dodoma Eva Mpagama, Monica Mtandu na Tuli Nasa.

Amesema kwa upande wa madiwani amepata jumla ya wanachama 70 ambao wanaomba kuteuliwa na chama hicho kupitia kata pamoja na wanawake 20 ambao wanaomba kuteuliwa kupitia udiwani viti maalum.

Katika Jimbo la Mtera amesema kuwa amejitokeza mtu mmoja tu ambaye ni Mratibu wa Chadema Kanda ya Magharibi, Christopher Nyamwanji ambaye amejitokeza kupimana ubavu na Livingstone Lusinde wa CCM.

Amesema kwa upande wa Madiwani wamepata jumla ya wanachama 15 wanaowania nafasi hiyo kwenye kata na viti maalum wamepata wanachama watatu tu.

Aidha amesema kuwa majina ya wanachama waliojitokeza kugombea udiwani na ubunge kwenye majimbo mengine saba yaliyosalia atayatoa baada ya kupata taarifa zao.