Jumatatu , 11th Mei , 2020

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeadhimia kuyapuuzia maagizo ya Spika wa Bunge la Tanzania Job Ndugai, aliyewataka Wabunge wote wa chama hicho ambao hawahudhurii vikao vya Bunge kwa sasa kurudisha posho walizolipwa, ambapo kwa umoja wao wanadaiwa zaidi ya Milioni 110.

Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika na Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai.

Taarifa hiyo imetolewa leo Mei, 11, 2020 na Katibu Mkuu wa Chama hicho John Mnyika, wakati akitoa taarifa ya maadhimio ya Kamati Kuu ya chama hicho, ambapo pamoja na mambo mengine kamati hiyo imeadhimia kuwafukuza uanachama Wabunge wake wanne, ambao ni Anthony Komu, Joseph Selasini, David Silinde pamoja na Wilfred Lwakatare.

"Ni juu ya madai yaliyotolewa na Spika kwamba, Wabunge wa CHADEMA waliopewa posho za kujikimu ni wezi, Kamati Kuu ya chama imelijadili jambo hili na imeamua kwamba madai ya Spika ni ya uongo na chama kimetoa rai kwa Wabunge kutokutekeleza yale ambayo Spika ameyaelekeza, ni kinyume na katiba ya nchi, sheria na utaratibu kwani Wabunge wa CHADEMA siyo wezi" amesema Mnyika.

Aidha CHADEMA wamesema kuwa watamuandikia barua haraka iwezekanavyo Spika Ndugai, ya kumjulisha juu ya kuwafuta uanachama Wabunge hao wanne ambao hadi sasa bado wanaendeleo na vikao vya BUnge.