Jumatatu , 13th Aug , 2018

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imehairisha Kesi inayowakabili viongozi wa ngazi za juu na Wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) leo, hadi Agosti 21, 2018 ambapo Mahakama hiyo itaweza kusikiliza maombi ya washtakiwa juu ya rufaa yao.

Nembo ya chama cha CHADEMA

Hayo yamebainishwa na washtakiwa namba 5 wa kesi hiyo ambaye ni Mbunge Tarime mjini Ester Matiko wakati akizungumza na www.eatv.tv, muda mchache yalipotolewa maamuzi hayo na kusema kwamba uamuzi huu umetokana na wakili wao kukata rufaa juu ya muendelezo wa kesi hiyo Mahakamani hapo.

"Kiukweli tunapata changamoto kubwa sana katika kesi hii kutokana na kuahirishwa mara kwa mara maana tunapoteza muda wetu mwingi sana. Lakini kwa upande mmoja naweza kusema ni njia moja wapo ya kutafuta haki ya kweli katika kesi yetu", amesema Matiko.

Hii ni mara ya nne mfufulizo kuhairishwa kesi inayowakabili viongozi wa CHADEMA kutokana na sababu mbalimbali zinazotolewa Mahakamani hapo wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo.

Itakumbukwa mnamo Julai 31, 2018 Mahakama ilihairisha kesi hiyo kutokana na kushindwa kufika Mahakamani kwa mshtakiwa Freeman Mbowe pamoja na Wakili wao, pia Agosti 2, 2018 hivyo hivyo kesi hiyo ilipigwa kalenda kwa mara nyingine kwa sababu ya mshtakiwa namba 5 ambaye ni Ester Matiko kupata dharula ya safari nje ya nchi.

Agosti 6, 2018 pia Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Wilbard Mashauri alihairisha kesi hiyo kutokana na  udhuru uliotolewa Mahakamani hapo kwa mawakili wa upande wa utetezi, kuwa Peter Kibatala na Jeremiah Mtobesya wameshindwa kufika mahakamani kutokana na kufuatilia kesi nyingine.

Viongozi wa CHADEMA wanaoshtakiwa ni pamoja na Mwenyekiti wao Freeman Mbowe, Katibu Mkuu wa chama hicho Dkt. Vicent Mashinji, Naibu Katibu Mkuu bara JohnMnyika, Naibu katibu Mkuu Zanzibar, Salim Mwalimu.

Wengine ni Mbunge wa Tarime vijijini John Heche, Mbunge Tarime mjini Esther Matiko, Mbunge wa Bunda mjini Ester Bulaya, Mbunge wa Iringa Mjini Peter Msigwa pamoja na Mbunge wa Kawe Halima Mdee.

Wote hao wanaandamwa na mashtaka 13 ikiwemo la kufanya mkusanyiko isiyokuwa na kibali kwenye chaguzi ndogo za marudio Jimbo la Kinondoni Jijini Dar es Salaam zilizofanyika Februari 17, 2018.