Jumatano , 25th Nov , 2020

Mkuu wa Idara ya Mawasiliano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tumaini Makene, amesema kuwa swali la kwamba wao wamesalitiwa na wabunge wa viti maalum walioapishwa jana, linapaswa liulizwe moja kwa moja kwa wabunge wenyewe kwa kuwa wao walipewa imani zaidi na wananchi.

Bendera za CHADEMA.

Kauli hiyo ameitoa hii leo Novemba 25, 2020, kwenye kipindi cha SupaBreakfast ya East Africa Radio, ambapo amesema kuwa hakukuwa na utaratibu wowote uliofanyika na kupelekea kupatikana kwa wabunge wa viti maalum kutoka ndani ya chama hicho.

'Hilo swali la kusalitiwa linawastahili wao vizuri akina (Halima Mdee, Esther Matiko, Ester Bulaya) wawaeleze wananchi waliokuwa wamewapatia imani kubwa kwa muda mrefu", amesema Makene.

Aidha Makene amesisitiza kuwa CHADEMA hakikufanya uteuzi wowote wala kuwasilisha majina ya wabunge wa viti maalum walionekana kuapishwa siku ya jana ya Novemba 24, 2020, jijini Dodoma.

"Hakukuwa na kitu chochote kinachoitwa uteuzi kwa maana ya chama kuketi katika vikao vyake, kwa mujibu wa katiba na kufanyia uteuzi na kuwasilisha hayo majina kwa mkurugenzi wa uchaguzi”, amesisitiza.

Jumla ya wabunge 19 wa viti maalum kupitia CHADEMA, walikula kiapo cha kulitumikia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akiwemo Halima Mdee,  Ester Bulaya, Esther Matiko na wengine.