Jumamosi , 14th Nov , 2020

Kamanda wa Polisi mkoa wa Simiyu, ACP Richard Abwao, amesema kuwa moto ulioteketeza nyumba aliyokuwa akiishi Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Meatu, Fabian Manoza, ulisababishwa na uwepo wa baadhi ya vifaa mbalimbali vya umeme vilivyokuwa vimechomekwa ikiwemo Friji.

Kamanda wa Polisi, mkoa wa Simiyu, ACP Richard Abwao.

Kauli hiyo ameitoa hii leo Novemba 14, 2020, wakati akizungumza na EATV&EA Radio Digital, kuelezea tukio la moto uliounguza nyumba hiyo, tukio ambalo limetokea usiku wa kuamkia leo na wakati nyumba inateketea Mkurugenzi huyo hakuwepo nyumbani, bali aliyekuwepo ni mdogo wake.

"Nyumba yote imeteketea kwa moto, nje kulikuwa na gari nalo kidogo liungue ila lilivutwa, na chanzo cha moto mule ndani, waliacha vitu vikiwa vimechomekwa kwenye umeme, ikiwamo friji, chaji za simu na vingine, nadhani umeme ulicheza ikatokea shida," amesema RPC Abwao.

Aidha Kamanda Abwao ameongeza kuwa wakati wa tukio hilo, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji walifika eneo la tukio, lakini wakashindwa kuuzima moto huo, "Mule ndani moshi mzito ulikuwa umetanda sana, hivyo zimamoto hawakuingia na hakuna madhara yoyote kwa binadamu na uchunguzi unaendelea ili kukibaini hasa kiini cha moto huo".