Jumamosi , 17th Nov , 2018

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameishukuru Serikali ya China kwa kuunga mkono jitihada za maendeleo zinazofanyika nchini hivi sasa chini ya uongozi wa Serikali ya awamu ya tano.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwa muwakilisha serikali ya China.

Ametoa shukrani hizo alipokutana na Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Watu wa China, Bw. Cai Dafeng ofisini kwake Mlimwa, jijini Dodoma.

Tunaishukuru Serikali ya China kwa sababu tumepokea misaada na mikopo ya gharama nafuu na kuendeleza miradi mbalimbali kama vile mradi wa umeme wa Kinyerezi, awamu ya pili ya ujenzi wa uwanja wa ndege wa Zanzibar,” alisema.

Tuna mahusiano mazuri kwenye sekta ya afya na sasa hivi tuna madaktari 20 ambao wanasoma huko na wengine wanasomea masuala ya TEHAMA. Pia tuna mahusiano mazuri baina ya Bunge la Tanzania na China,” alisema.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Watu wa China, Bw. Cai Dafeng alisema amefurahishwa na jinsi Serikali ya awamu ya tano inavyoendelea kubadili hali ya uchumi wa nchi na maisha ya Watanzania chini ya uongozi wa Dkt. John Pombe Magufuli.

Akizungumzia kuhusu masuala ya uwekezaji baina ya Tanzania na China, Bw. Cai alisema China itaendelea kuyahimiza makampuni ya nchi hiyo ili yawekeze zaidi nchini Tanzania kwenye maeneo mbalimbali kama vile ujenzi wa bandari ya Bagamoyo. “China inataraji kuongeza uwekezaji kwenye kilimo, nishati na miundombinu,” alisema.

Kuhusu elimu, Bw. Cai alisema Serikali ya nchi hiyo inaangalia uwezekano wa kuanzisha masomo ya lugha ya Kichina katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ili Watanzania wengi zaidi waweze kujifunza lugha hiyo.