Jumatatu , 13th Aug , 2018

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imemtangaza Mhandisi Christopher Chiza kutoka CCM kuwa mshindi wa kiti cha Ubunge katika Jimbo la Buyungu Mkoani Kigoma baada ya kupata jumla ya kura 24,758 akifutiwa na Elias F. Michael aliyepata kura 16,910 kutoka CHADEMA.

Mhandisi christopher Chiza

Hayo yamebainishwa na msimamizi wa uchaguzi jimboni humo Lusubilo Mwakabibi ambapo amesema watu waliojiandikisha kupiga kura walikuwa 61,980 na kura zilizopigwa zilikuwa 42,356 huku zikiharibika kura 515.

Matokeo hayo yametokana na uchaguzi mdogo wa marudio uliofanyika jana Jumapili Agosti 12, 2018, katika Mkoa huo kufuatilia jimbo hilo kuwa wazi.

Licha ya matokeo hayo kutangazwa, mgombea kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), amedai hakutendewa haki kutokana na kunyimwa baadhi ya fomu za matokeo na kutokubaliwa kuingia katika chumba cha kuhesabia kura, huku akidai zaidi kuwa yeye alishinda kwa kura 22,000 huku Chiza akiwa amepata kura 18,000.

Kwa upande wake mshindi wa nafasi kiti hicho cha Ubunge, Mhandisi Christopher Chiza amewashukuru wananchi wa Kigoma kwa kuweza kumuamini kuwa mwakilishi wao Bungeni kwa mara nyingine tena.

Mhandisi Chiza ambaye ni mshindi wa jimbo hilo kwa sasa pia aliwahi kulitumikia jimbo hilo kwa takribani miaka 10 iliyopita, kuanzia mwaka 2005 hadi 2015 kupitia CCM, ambapo alikuja kuangushwa katika uchaguzi wa Rais na Wabunge wa mwaka 2015  na marehemu Kasuku Bilago aliyekuwa CHADEMA.

Mnamo Julai 10, 2018, Katika kikao cha Kamati Kuu ya CCM kilichokuwa kinaongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho Taifa ambaye pia ni Rais wa Tanzania, Dkt. John Magufuli, walimteua Mhandisi Christopher Kajoro Chiza kuwa mgombea wa Ubunge katika Jimbo la Buyungu.

Uchaguzi huo wa marudio umefanyika baada ya kufuatia aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kupitia tiketi ya Chadema, Kasuku Samson Bilago kufariki dunia mnamo Mei 26, 2018, katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) alikokuwa amelazwa kwa matibabu na kupelekea jimbo hilo kuwa wazi.