Jumamosi , 21st Sep , 2019

Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Bi. Zainabu Telack, ametoa tahadhari kwa wananchi wa eneo la Ndembezi Mazinge, mkoani humo, kutokana na uwepo wa dalili za Volcano.

Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Bi. Zainabu Telack

Akiongea na EATV & EA Radio leo Bi. Zainabu Telack, amesema kuwa amewataka wakazi wa eneo hilo lililopo Kata ya Ndembezi nje kidogo ya Manispaa ya Shinyanga, kukaa mbali ili kuepuka kupata madhara endapo hali hiyo ikiwa sio ya kawaida.

'Hili eneo linaonekana kama lava au Volcano, lakini hatujathibitisha bado maana udondo unaotoka ni wa baridi, sasa isije kutokea udondo wa moto ukaleta madhara', ameeleza.

Aidha mkuu huyo wa mkoa ameongeza kuwa, 'Hili suala lipo kwa wiki ya pili sasa na ni karibu kiasi na makazi ya watu lakini Watalaamu wa Jiolojia walikuja na hawakubaini madhara yoyote lakini leo (Septemba 21, 2019), kuna watalaamu wanaingia wao ndio watatueleza zaidi'.

Kuhusu mazingira ya eneo, RC amesema kuwa ni kilima ambacho sio kikubwa sana lakini kimekuwa kikitoa udondo tepetepe, ambao unatoka chini kupanda juu lakini kwa mujibu wa wazee wa zamani katika eneo hilo, hicho kitu si cha kawaida kihistoria.