"Dar es Salaam kuna mapungufu, RC yupo"- Magufuli

Jumatatu , 18th Jan , 2021

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Magufuli, amesema kuwa atakaporudi Dar es Salaam, akute ujenzi wa shule ya msingi Barango, iliyopo wilayani Ubungo iwe imekamilika na wanafunzi wawe wanakaa kwenye madawati.

Kushoto ni Rais Dkt. John Magufuli na kulia ni Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaa, Aboubakar Kunenge

Agizo hilo amelitoa hii leo Januari 18, 2021, mjini Bukoba, mkoani Kagera mara baada ya kufungua shule ya wavulana ya Ihungo iliyopo mkoani humo , ambapo ameshangaa kuona viongozi ndani ya mkoa huo wapo akiwemo Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Aboubakar Kunenge na kuongeza kuwa hali hiyo inaonesha kuwa alikosea kuchagua viongozi.

"Hata Dar es Salaam kuna mapungufu kuna shule moja ya msingi Ubungo inaitwa Barango, ina wanafunzi wengi tu na bado wanakaa chini madarasa mengine yamebomoka, madawati yamevunjika na yameachwa bure, Mkuu wa wilaya yupo, Mkuu wa mkoa yupo, Mkurugenzi na mbunge wa Ubungo yupo na ni Profesa wa Elimu lakini hiyo shule wanafunzi wanakaa chini", amesema Rais Magufuli.

Aidha Rais Magufuli ameongeza kuwa, "Ninamshukuru mwandishi ameitoa kwenye mitandao na viongozi wa kule wakaanza kusema ni masuala ya kisiasa hayo si masuala ya kisiasa hayo ndiyo mimi ninapenda kuyajua, ninazungumza nikiwa Kagera lakini nikienda Dar es Salaam nikute madarasa yamekamilika na wanafunzi hawakai chini, nitaenda kuitembelea kama wananisikia wa Dar es Salaam, Message sent and Delivered".