Daraja lililopewa siku 7 na JPM lilivyoua watano

Jumanne , 24th Mar , 2020

Watu watano wamefariki Dunia na wengine sita kujeruhiwa, kufuatia ajali ya barabarani baada ya Lori kubwa la mizigo, kuigonga gari ndogo ya abiria aina ya Noah, wakati likisubiri kuvuka katika daraja la mchepuko la kiyegeya, ambalo lilisombwa na maji mwanzoni mwa mwezi Machi.

Gari ndogo aina ya Noah iliyokuwa imebeba abiria,ikiwa imepondeka vibaya.

Ajali hiyo imetokea usiku wa kuamkia Machi 23, 2020, huku chanzo kikielezwa kuwa ni kufeli kwa breki ya Lori na kupelekea vifo vya watu wanne papo hapo na mmoja kufariki wakati akipatiwa matibabu hospitalini.

Akizungumza katika eneo la tukio Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro Wilbroad Mutafungwa, ameeleza kuwa gari hiyo ndogo ilikuwa imebeba abiria kutoka Dumila kuelekea Gairo na kwamba Jeshi la Polisi linaendelea kumtafuta dereva wa Lori kwani alikimbia.