Jumatano , 18th Feb , 2026

Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tundu Lissu, imeendelea leo katika Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam, huku Shahidi wa siri wa 11 akitoa ushahidi unaohusu madai ya mpango wa Tundu Lissu wa kutaka kuzuia uchaguzi mkuu wa mwaka 202

Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tundu Lissu, imeendelea leo katika Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam, huku Shahidi wa siri wa 11 akitoa ushahidi unaohusu madai ya mpango wa Tundu Lissu wa kutaka kuzuia uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Shahidi huyo, aliyetambulika kwa jina la P7 kwa sababu za kiusalama, aliiambia mahakama kuwa ni dereva bajaji kutoka Arusha na kwamba amekuwa akijishughulisha na kazi hiyo tangu mwaka 2023.

Alidai kuwa alimsikia mshitakiwa akitoa kauli zinazohamasisha kuzuia uchaguzi mkuu wa mwaka jana, akisema kuwa polisi wanaiba kura na kwamba mahakama haziwezi kutoa haki kwa kuwa majaji ni “vibaraka wa CCM”.

Kwa mujibu wa shahidi, kauli hizo zilimshawishi yeye pamoja na wengine kuunga mkono wito wa kuzuia uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, akieleza kuwa walichochewa pia na hali ngumu ya maisha.

Hata hivyo, shahidi alieleza kuwa baadaye watu waliojitambulisha kama maafisa wa polisi waliwakamata yeye na kijana mwingine P4, wakidaiwa kufanya fujo.

Katika hatua ya maswali ya dodoso kutoka kwa Mshtakiwa Tundu Lissu, alimhoji shahidi kuhusu maudhui ya maelezo yake, akimtaka athibitishe iwapo baadhi ya kauli alizozitaja mahakamani zilikuwepo katika maelezo yake ya awali. Shahidi alikiri kuwa baadhi ya maneno, ikiwemo madai ya kauli ya “watakinukisha sana”, hayakuwepo katika maelezo aliyoyaandika polisi.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa madai kuhusu polisi kuiba kura na kutopatikana kwa haki mahakamani yaliandikwa katika maelezo yake.

Alipoulizwa iwapo kumuunga mkono mshitakiwa katika wito wa kuzuia uchaguzi ni kosa la jinai, shahidi alisema hana uhakika. Lakini alikubali kuwa kuzuia uchaguzi ni kosa kisheria, akisema ndiyo sababu walikamatwa ingawa hakuwahi kufikishwa mahakamani kwa shtaka hilo.

Tofauti kati ya maelezo yaliyoandikwa polisi na ushahidi wa shahidi mahakamani zimeibuliwa wakati wa usikilizwaji huo.