Jumapili , 6th Sep , 2020

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Dkt Bashiru Ally, amemtaka mgombea Ubunge wa Jimbo la Nzega Vijijini Dkt Hamis Kigwangalla, kuacha kujibizana mitandaoni kuhusu mpira na badala yake, atumie muda huo kuweka vitu vitakavyomsaidia mgombea Urais wa chama hicho Dkt Magufuli kushinda uchaguzi.

Katibu Mkuu wa CCM Dkt Bashiru Ally

Hayo yameelezwa hii leo Septemba 06,2020, kupitia ukurasa wa Twitter wa CCM, ambapo licha ya kutoa maelekezo hayo kwa Kigwangalla, pia ametoa maelekezo kwa mgombea Ubunge wa Jimbo la Mtama Nape Nnauye.

"Naona Dkt Kigwangalla yupo mitandaoni kujibizana na Mohamed Dewji mambo ya mipira, tupo kwenye uchaguzi, nataka nione ana-tweet na wafuasi wake namna Mwenyekiti na Mgombea Urais wetu atakavyoshinda, siingilii maisha binafsi, hakuna maisha binafsi unapokuwa mgombea wa CCM" amesema Bashiru.

Dkt Bashiru pia akatoa maelekezo haya kwa Nape, "Nimemuona Nape Ilemela, wakati Jakaya kikwete anakwenda Lindi Septemba 8, 2020 kuzindua, anatakiwa awe Lindi kumuandalia Mkutano,tutakuwa wakali kusimamia nidhamu, wagombea wa CCM wapo chini ya Kamati za Siasa, lazima wafuate maelekezo, sio kujiamulia binafsi" ameongeza Dkt Bashiru.

Mbali na hayo Dkt Bashiru ameongeza kuwa, "Hakuna Mgombea yeyote kutoka Jimboni kwake bila idhini ya Kamati ya Siasa ya Wilaya, tufuate ratiba za NEC na  Kamati za Siasa, tuwatafutie kura wagombea Udiwani na Mgombea Urais, tufafanue Ilani yetu tuliyotekeleza na kilichobaki, na kuhamasisha wananchi kupiga kura"