Ijumaa , 21st Feb , 2020

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli, ameeleza ni kwa namna gani amefurahishwa kukutanishwa pamoja tena na Madaktari kwani anaitambua kazi yao kubwa ya kuhudumia watu katika jamii.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli na Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt Zainabu Chaula.

Rais Magufuli ameyabainisha hayo wakati akizungumza na Madaktari na Wauguzi, wakati wa maadhimisho ya siku ya Madaktari Kitaifa, na ndipo alipoeleza ni kwa namna gani anaukumbuka mchango wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt Zainabu Chaula.

"Mimi nina historia nzuri na Madaktari, nakumbuka siku moja nikiwa Naibu Waziri nilienda kutolewa jino Muhimbili, niliamka baada ya siku mbili nikiwa ICU, pia nilishawahi kuwa ICU Dodoma, nikaamka nikakuta nahudumiwa na Dkt Zainabu, kwahiyo Dkt Zainabu ananijua kila kitu ingawa mimi simjui kila kitu". amesema Rais Magufuli.

Aidha Rais Magufuli ameahidi, kuzitatua changamoto zote zilizobainishwa na Madaktari kwa lengo la kuhakikisha huduma bora za afya zinaendelea kutolewa.