Jumatano , 2nd Dec , 2020

Jeshi la Polisi mkoa wa Geita, linawashikilia watu watatu wa familia moja kwa tuhuma za kumuuwa mama yao Selestina Manyanda (70), mkazi wa Kijiji cha Nyaruyeye, baada ya kumpiga na vitu vyenye ncha kali mwilini mwake kwa sababu ya kuwanyima ardhi ya kuchimbia madini ya dhahabu.

Kamanda wa polisi mkoa wa Geita, Henry Mwaibambe.

Taarifa hiyo imetolewa leo Disemba 2, 2020, na Kamanda wa Polisi mkoani humo Henry Mwaibambe, na kusema kuwa tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia Disemba 1 mwaka huu, ambapo pia amekitaja chanzo cha mauaji hayo kwamba familia hiyo ina mgogoro mkubwa juu ya namna ya kugawana eneo hilo.

"Familia ina ugomvi mkubwa sana hasa katika eneo la uchimbaji ni namna ya kugawana eneo la kuchimba, hili ni tukio baya na huyu mwanamke mume wake ana miaka 90 nadhani walichukulia advantage kwamba wote ni wazee hawana uwezo wa kujisaidia lakini wote waliweza kutambuliwa na tunawashikilia", amesema Kamanda Mwaibambe.

Aidha jeshi hilo pia, linamtafuta Masolwa Sangesange , kwa tuhuma za kumshambulia kwa kumkata na mapanga mwanaye wa kumzaa anayejulikana kwa jina la Jumanne Masolwa, baada ya mtoto huyo kuuza kuku wake anaowafuga mwenyewe kwa lengo la kuendeleza bustani yake na ndipo baba yake alimpofanyia ukatili huo.