Jumatatu , 19th Sep , 2022

Familia ya mtoto aliyefariki dunia, Bennet Laurence Kiwelu mwanafunzi wa darasa la 5 Shule ya Msingi Mount Sayuni ya Dar es Salaam kwa kile kilichodaiwa kuwa ni baada ya kushambuliwa na mwalimu shuleni Jumatatu iliyopita, imesema kuwa taarifa hizo siyo za kweli.

Bennet L. Kiwelu, Mwanafunzi aliyepoteza maisha

Dkt. August Mtui ambaye ni mjomba wa marehemu na Daktari wa binadamu kwa niaba ya familia amesema kwamba, kwamujibu wa matibabu na vipimo alivyofanyiwa marehemu pamoja na historia yake ya afya, zinaashiria kwamba Bennet alikuwa na tatizo la kiafya kichwani ambalo limepelekea kifo chake baada ya kuzimia akiwa shuleni, na kwamba hakuna uhusiano na adhabu ya shuleni kama inavyosambazwa kwenye mitandao na makundi ya WhatsApp.

“Siku ya jumatatu iliyopita baba mzazi wa Bennet ambaye ni shemeji yangu alinipigia SIM kwamba mpwa wangu amezimia akiwa shule na amepelekwa hospital, nilifika hospital pamoja na shemeji yangu lakini bado ilionekana anatatizo la kupumua ambapo alikimbizwa hospitali ya Muhimbili na huko baada ya kipimo cha cityscan ilionekana kuwa damu inavujia kwenye ubongo baada ya mshipa kupasuka kisha akafariki alfajiri ya Septemba 18. Hivyo kutokana na uchunguzi huo ni kwamba siyo kweli kwamba Bennet alishambuliwa shuleni, na Walimu hawajahusika kwa lolote hapa ni tatizo tu la kiafya ambalo inaonekana alikuwa nalo.”- Dkt. August Mtui,  Mjomba wa Marehemu.

Kutokana na tukio hilo pamoja na uvumi uliosambazwa kwenye mitandao na makudi ya WhatsApp,  Meneja wa Shule ya Mount Sayuni amewaomba raia kupuuza uvumi huo.

“Bennet alipiga kelele darasani siku ya jumatatu iliyopita na tulivyoenda tulimkuta akilalamika maumivu ya kichwa na jicho. Lakini baada ya kumpatia huduma ya kwanza tulimtafuta mzazi wake na tukamkimbiza hospitali ambapo baadaye alipelekwa Muhimbili na bahati mbaya amefariki. Ukweli wa sababu ya kifo chake kama walivyoeleza wazazi ni matatizo katika mishipa ya ubongo na siyo kama inavyoenezwa kwamba alipigwa shuleni, siyo kweli na kama ingekuwa hivyo basi ingeonekana kitaalam.”- Christopher Sempamba, Meneja Shule ya Mount Sayuni.
 
Kwa mujibu wa familia, Mwili wa Bennet Laurence Kiwelu utasafirishwa jumatano kuelekea Moshi ambapo siku ya Alhamisi mazishi yatafanyika Marangu, Kilimanjaro.