Familia yataja eneo atakalozikwa Waziri Simba

Ijumaa , 14th Feb , 2020

Msemaji wa Familia ya Marehemu Idd Simba, Ahmed Simba, amesema kuwa mwili wa Waziri wa zamani wa Viwanda na Biashara, utapumzishwa katika makaburi ya Mwinyi Mkuu Magomeni, lengo likiwa ni kumpumzisha mahali ambapo Baba zake wote walizikwa.

Marehemu Iddi Simba na Waziri wa Zamani wa Viwanda na Biashara, wakati wa uhai wake.

Akizungumza na EATV&EA Radio Digital leo Februari 14, 2020, Ahmad amebainisha kuwa kwa sasa bado wako nyumbani wakijiandaa kwa ajili ya kwenda Msikitini wa Manyema kuuswalia mwili huo.

"Sasa hivi tuko hapa Msasani nyumbani kwake, tutaondoka na mwili mpaka Msikiti wa Manyema utaswaliwa pale kisha tutaelekea Magomeni na atazikwa katika makaburi ya Mwinyi Mkuu, anazikwa kule kwa sababu Baba zake wote wamezikwa hapo" amesema Ahmad.

Waziri wa zamani wa Viwanda na Biashara Iddi Simba, alifariki Dunia siku ya jana Februari 13, 2020, katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete alikokuwa akipatiwa matibabu, ambapo alihudumu nafasi yake kati ya mwaka 2001 na 2002.