Ijumaa , 12th Sep , 2025

Waandamanaji walisema wanadai heshima ya kitaifa kwa wapendwa wao na hawajapendezwa na fidia ya kifedha.

 Familia za waandamanaji waliouawa na polisi nchini Nepal zimekusanyika jijini Kathmandu siku ya jana Alhamisi, zikionyesha hasira dhidi ya mamlaka na kutafuta taarifa kuhusu ndugu zao waliopotea.

Failia hizo zimefanya ibada ya mishumaa nje ya chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali jijini humo na kutangaza mpango wa kukutana na maafisa wa jeshi la Nepal ili kudai haki. Mapema siku hiyo, mamia ya watu walijazana katika uwanja mkuu wa ndege wa Nepal uliopo Kathmandu wakijaribu kuondoka nchini humo, huku mkanganyiko ukiibuka kuhusu nani anayeongoza taifa la Himalaya baada ya maandamano ya vurugu kuipindua serikali ya nchi hiyo.

“Tunahitaji kupigania haki kwa familia zetu na ndugu zetu waliouawa na hatuwezi kubaki kimya tena,” alisema Kamal Subedi, mmoja wa waliokuwepo kwenye ibada hiyo ya mishumaa ambaye mpwa wake aliuwawa. “Tumepoteza wapendwa wetu lakini siasa zinaonekana kupewa kipaumbele na hakuna mtu hata mmoja aliyetufikia, hivyo sasa tunapigania haki na heshima wanayostahili ndugu zetu.”

Waandamanaji walisema wanadai heshima ya kitaifa kwa wapendwa wao na hawajapendezwa na fidia ya kifedha. Maandamano ya siku kadhaa yalimlazimu Waziri Mkuu Khadga Prasad Oli kujiuzulu siku ya Jumanne, akimwomba Rais wa heshima wa nchi hiyo, Ram Chandra Poudel, kuongoza serikali ya mpito hadi serikali mpya itakapoundwa. Taarifa zinasema Oli alikimbia makazi yake rasmi, na haijulikani alipo.

Wakazi wa mji mkuu wamebaki wakijiuliza ni nani hasa aliyeko madarakani. Anup Keshar Thapa, afisa wa serikali mstaafu aliyekuwa akiangalia makazi rasmi ya mawaziri yaliyoteketea, alisema haikuwa wazi ni nani ataiongoza nchi na iwapo wananchi wangeweza kuwasikiliza. “Kama maandamano yangelikuwa yamepangwa kwa utaratibu, ingekuwa wazi ni nani anayeyaongoza,” alisema.

Viongozi wa maandamano walikutana na maafisa wa jeshi katika makao makuu ya jeshi mjini Kathmandu siku ya Jumatano kujadili kuhusu kiongozi wa mpito.