Jumamosi , 14th Mei , 2016

Waziri Mkuu Mstaafu Fredrick Sumaye ameteuliwa kuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) akiwa ni mjumbe wa pili kuteuliwa na Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe.

Waziri Mkuu Mstaafu Fredrick Sumaye ameteuliwa kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) akiwa ni mjumbe wa pili kuteuliwa na Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe baada ya waziri mkuu mstaafu na mgombea urais kupitia chama hicho mwaka 2015 Edward Lowassa.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salimu Mwalimu amesema kuwa uteuzi huo umefanywa kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho kipengele 7.7 (14) ya mwaka 2006.

Amesema kuwa katiba hiyo inampa Mwenyekiti mamlaka ya kuteuwa wajumbe sita kwa kadiri atakavyoona inahitajika na kwamba kwa mamlaka hayo ndiyo ameweza kumteuwa Sumaye kuwa mjumbe wa Kamati Kuu kutokana na uhitaji ulivyo hivi sasa.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Bara wa Chadema John Mnyika alisema kuwa chama hivyo hakina wasiwasi na wajumbe hao kuwa wanaweza kukiharibu chama chao kwa kuwa wana mikakati madhubuti ya kuzuia masuala yote ya usaliti na hujuma kwenye chama hicho.