Jumanne , 23rd Dec , 2025

Boniventure alifariki dunia Disemba 22, 2025 saa 6:30 mchana akiwa anaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali Teule ya Ifisi.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia Furaha Mwile Nyelele, mkazi wa Kijiji cha Shilanga kwa tuhuma za mauaji ya mtoto wa jirani yake aliyekuwa Mwanafunzi wa Shule ya Msingi Shilanga darasa la saba aitwaye Boniventure Elia Lazaro (12) mkazi wa Shilanga.

Taarifa iliyotolewa na Imetolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya leo Disemba 23,2025 imeeleza kuwa, awali kabla ya tukio hilo tarehe 21 Disemba 2025 majira ya saa 10:15 jioni huko Kijiji cha Shilanga, Kata ya Ilembo, Tarafa ya Isangati, Wilaya ya Mbeya Vijijini mtuhumiwa Furaha Mwile Nyelele alimpiga kwa kipande cha mti kichwani mtoto Boniventure Elia Lazaro (12) ambaye kwa sasa ni marehemu na kumsababishia jeraha ambapo alikimbizwa katika Hospitali Teule ya Ifisi kwa matibabu.

Boniventure alifariki dunia Disemba 22, 2025 saa 6:30 mchana akiwa anaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali Teule ya Ifisi.

Uchunguzi wa awali wa Polisi umebaini kuwa chanzo cha tukio hilo ni kujichukulia sheria mkononi baada ya mtuhumiwa kumtuhumu mtoto kuiba mayai ya kuku.

Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi limetoa wito kwa jamii kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi ili kuepuka madhara. Aidha, limewakumbusha wazazi na walezi kuzingatia suala la ulinzi na usalama wa mtoto kwa kuhakikisha haki za mtoto zinaheshimiwa na kulindwa.