Jumanne , 4th Feb , 2020

Umoja wa Wavuvi wa Samaki wa mkoani Mara na mkoa jirani wa Mwanza wamelalamikia vitendo vya ujambazi vinavyofanywa na baadhi ya wavuvi wenzao wanaovaa sare za polisi wa Uganda na kuvamia wenzao na kupora mali zao.

Wavuvi wakiwa majini

Hayo yamejiri wakati wa kikao cha kamati ya ulinzi na usalama   za mikoa yote miwili  na wadau wa uvuvi wa pande zote kilichofanyika mkoani Mara na kutanabaisha kuwa wizi huo umekuwa kwa kasi kwani wavuvi wanaibiwa na kuuawa huku samaki wakitoroshwa kwa magendo.

"Kuna wavuvi Watanzania wanavaa sare za Uganda, wanatunyang'anya mitumbwi. Kuna bwana mmoja juzi alinyang'anywa mtumbwi na askari waliovaa sare hizo na walipokutana askari wa Uganda wakawaeleza hilo", amesema Rajabu Ndonyi, mmoja wa wavuvi.

Kwa upande wao wakuu wa wilaya ya Musoma na Ukerewe kwa pamoja wamekemea vitendo hivyo na kuahidi kuchukua hatua stahiki kwa yeyote atakayekamatwa.