Jumatano , 9th Mar , 2016

Wananchi wa mikoa ya Mtwara na Lindi wametakiwa kujiandaa na kupanda kwa gharama za kuvuta umeme majumbani (Service line) zitakazofikia kiasi cha sh. 177,000 kama maeneo mengine kutoka sh. 99,000 ya sasa.

Mafundi wakiwa katika mitambo ya Umeme

Akizungumza na East Africa Radio ofisini kwake, Mhandisi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoa wa Mtwara, Daniel Kyando, amesema punguzo hilo ilikua ni ofa maalumu ambayo ifikapo Machi 31 mwaka huu itafikia mwisho, hivyo watakohitaji kuunganishiwa umeme baada ya hapo watalipia gharama halisi.

Aidha, amewaondoa hofu wananchi hao kutokana na hali ya kukatika kwa umeme mara kwa mara inayoendelea na kudai kuwa hali hiyo inatokana na marekebisho ya miundombinu ikiwamo nguzo pamoja na matengenezo makubwa ya mtambo mmoja ambao uliharibika kutokana na kuanguka kwa nguzo.

Amesema, wananchi wasiwe na wasiwasi kwani huduma hiyo itarejea katika hali yake ya kawaida ndani ya wiki hii kwasababu vifaa vilivyokuwa vikihitajika kwa ajili ya matengenezo ya mtambo huo tayari vimewasili.