Gondwe aingilia kati kumsaka dereva aliye'overtake

Jumatano , 14th Aug , 2019

Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe ameliagiza jeshi la polisi mkoa wa Tanga kumsaka kokote kule aliko dereva wa basi la Buffalo aliyesababisha ajali baada ya ku'overtake' eneo lisiloruhusiwa.

Gondwe ametoa agizo hilo leo Agosti 14 mara baada ya kutokea kwa ajali iliyohusisha basi lililokuwa na abiria takribani 45 na gari ndogo katika kijiji cha Kwekwale wakati likitokea Arusha kuelekea Dar es Salaam na hakuna kifo chochote kilichotokea.

''Naliagiza jeshi la polisi kumtafuta dereva wa hili basi,  halafu ashtakiwe kwa kosa la ku 'overtake' sehemu ambayo alama haziruhusu kufanya hivyo'', amesema DC Gondwe.

Ajali hiyo imetokea baada ya dereva wa basi kutaka kuyapita magari mawili yaliyokuwa mbele yake na ndipo alipovaana uso kwa uso na dereva wa gari ndogo yenye namba za usajili T 706 DPE mali ya Lucas Karoli ambapo abiria waliokuwepo kwenye basi hilo wametafutiwa gari nyingine na kuendelea na safari.