Hatma ya Mbunge CCM aliyemgomea Spika Ndugai

Jumatatu , 20th Mei , 2019

Leo May 20, 2019 Mbunge wa Shinyanga Mjini Stephen Masele anatarajiwa kuhojiwa na Kamati ya Maadili ya Bunge kufuatia kutuhumiwa kuendeleza vitendo vya utovu wa nidhamu na kuwachonganisha viongozi wa Serikali na Bunge.

Mbunge wa Shinyanga Mjini Stephen Masele.

Mbunge huyo amewasili nchini mwishoni mwa juma lililopita akitokea nchini Afrika Kusini alipokuwa akilitumikia Bunge la Afrika (PAP), ambapo alikuwa kwenye mgogoro na Rais wake, Roger Dang ambaye alituhumiwa kwa matumizi mabaya ya madaraka.

Akizungumza na vyombo vya habari mwishoni mwa juma lililopita, Spika Ndugai alimtaka kiongozi huyo kufika kuhojiwa kwenye Kamati ya Maadili ya Bunge Jumatatu majira ya saa 5 asubuhi.

Akizungumzia na wanahabari, Spika Ndugai alisema kuwa, "Stephen Masele hawezi kukaidi zaidi kwa sababu ni lazima arudi Tanzania, labda awe mkimbizi na akirudi lazima aje Kamati ya Maadili, tunachomuitia ni tabia yake ya uchonganishi wa viongozi, hatuwezi kusema ila mtaelewa fitina ikoje, ambayo ni kukosa sifa kwa kiongozi".

Lakini Stephen amebainisha ataweka kila kitu wazi mbele ya waandishi wa habari juu ya kilichotokea mpaka kumfikisha kwenye kikao cha nidhamu cha kamati ya maadili ya Bunge.