Jumatatu , 3rd Dec , 2018

Meya wa Jiji la Dar es salaam kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, Isaya Mwita, ameachiwa kwa dhamana baada ya kushikiliwa kwa tuhuma kufanya maandamano bila kibali.

Meya wa Jiji la Dar es salaam kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, Isaya Mwita.

Mwita ambaye pia ni diwani kata ya Kigamboni alikamatwa na Jeshi la Polisi jumamosi ya Disemba mosi saa 11 jioni baada ya kumaliza kikao cha kutunisha mfuko wa vijana na kuachiwa usiku wa kuamkia leo.

Akizungumza Jijini Dar es salaam wakili wa Meya huyo, Alex Massaba amesema baada ya polisi kuchukua maelezo walimuachia kwa dhamana na kumtaka afike leo.

Mteja wangu amepata dhamana jana saa mbili usiku baada ya kuhojiwa kwa kosa la kufanya maandamano bila kibali na kutakiwa kuripoti kwa mkuu wa upelelezi wilaya ya Kigamboni leo,” amesema Massaba.

Hivi karibuni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dar es salaam Lazaro Mambosasa, alipiga marufuku kwa taasisi na idara mbalimbali kufanya maandamano bila kibali.

"Jeshi la polisi linatoa onyo kwa wanaoandamana bila kibali ikiwemo wizara, idara za serikali, NG’O na taasisi zozote zilizosajiliwa kisheria kuacha kufanya maandamano bila kutoa taarifa ili jeshi la polisi liweze kutoa ulinzi" alisema Mambosasa