Jumamosi , 4th Mei , 2024

Hivi karibuni dunia imeshuhudia hali ya hewa isiyotarajiwa ikitokea katika baadhi ya nchi duniani hususani Barani Afrika ikiwemo Mvua za kuzidi wastani ambazo hazikutaratiwa na kusababisha maafa na vifo.

Sehemu ya Ardhi iliyoathirika na Mabadiliko ya Tabia Nchi

Katika ripoti ya jukwaa la uchumi duniani  ya mwaka 2024 inayojulikana kama (WEF global risk )moja ya mambo ambayo  yameelezwa ni pamoja na namna hatari za maswala ya mazingira zinavyoendelea kuwa janga kubwa zaidi duniani huku wataalamu wengi wakiwa na wasiwasi kuhusu matukio mabaya zaidi kuhusu hali ya hewa yanayoweza kutokea duniani .

Je ni  kwanini hali hii inatokea sasa?
 
Wataalam wa hali ya hewa duniani wengi wanasema  hili ni jambo ambalo limetokana na athari ya mabadiliko ya tabia nchi jambo ambalo limekuwa likijadiliwa na viongozi kuagalia namna wanaweza kulitafutia suluhu.lakini zipo sababu nyingine ambazo zimekuwa zikisababishwa na wananchi wenyewe kutokana na shughuli za kila siku na miongoni mwa sababu hizo ni pamoja na :-
 
Ongezeko la taka zisizotunwa vizuri:
Kwa mujibu wa Dkt. Edmund Mabuye kutoka kitivo cha mabadiliko ya tabia nchi chuo kikuu cha Dar es salaam anasema ongezeko la taka sisizotunzwa vizuri ama hazikuwekwa eneo ambalo linasababisha taka kupelekwa maeneo ambayo yasiyo takiwa.

“Ongezeko la taka ambazo hazitunzwi vizuri au haziwekwi kwenye maeneo ambayo hayawezi kuathiri miundombinu ya kupeleka maji maeneo ambayo hayawezi kuleta madhara ”.Amesema Dkt. Edmund
 
Anaongeza pia ujenzi wa miundombinu ambayo inajengwa wakati mwingine haizingatii taarifa za mwenendo wa hali ya hewa kwa hali ambayo imepita,iliyopo na hata ile ambayo inakuwa imetabiriwa na hivyo majanga ya hali ya hewa yanapotokea yanakuwa na madhara makubwa.
 
Maendeleo ya viwanda duniani:
Viwanda duniani vimekuwa vingi na vimekuwa vikisababisha ongezeko la gesi joto duniani jambo ambalo limekuwa na madhara makubwa katika utunzaji wa mazingira duniani na athari zake zimekuwa zikijitokeza kwa njia za mafuriko ama ukame .
 
Ongezeko la kasi la watu.
Bi Mary ambaye ni mtaalam wa mazingira anasema miongoni mwa sababu kubwa la mabadiliko hayo ya tabia nchi na kufanya mvua zinazonyesha kuwa namadhara makubwa zaidi kwa jamii hususani barani Afrika ni kutokana na ongezeko kubwa la kasi la watu na ambalo limefanya watu kufanya ujenzi holela usiofuata kanuni za mazingira ikiwemo ujenzi wa kuzuia na kukinga njia za maji na hivyo kile tunachoona sasa maji yamekosa njia yake ya kawaida na hivyo yanatafuta njia mbadala na kuishia kwenye majumba ya watu na kuishia kuwa mafuriko.
 
Serikali za Afrika zifanye nini kunusuru majanga ya hali ya hewa.
Katika mazngumzo yangu na Dr Edmund anasema kunahitajika nguvu ya pamoja katika mataifa barani Afrika kuhakikisha mamuzi yanayofanywa yanakuwa na tija hususani katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi
 
“Viongozi wan chi mbalimbali inabidi waanze kuelewa kuwa suala la mabadiliko ya Tabia nchi ni janga ambalo linahitaji umakini katika sera mbalimbali nchini”.Amesema Dr Edmund Mabuye mtaalamu wa mazingira kutoka kitivo cha mabadiliko ya tabia nchi chuo kikuu cha Dar es salaam
 
Nchini Tanzania katika kuhakikisha wanakabiliana na madhara yatokanayo na hali ya hewa isiyotarajiwa ikiwemo mvua za kuzidi kiwango, ukame na majanga mengine kama maporomoko ya udongo wameanza mchakato wa kuimarisha upatikanaji wa taarifa za hali ya hewa hadi ngazi za mitaa.