Alhamisi , 26th Nov , 2020

Aliyekuwa mbunge wa jimbo la Mbeya Mjini, kupitia CHADEMA, Joseph Mbilinyi, amesema yeye hana mamlaka ya kumkabidhi ofisi mbunge wa sasa wa jimbo hilo kupitia CCM Dkt. Tulia Ackson, kwani ofisi aliyokuwa akiitumia, alikwisharudisha funguo kwa mamlaka husika na kwamba amuache na achape kazi

Kushoto ni aliyekuwa mbunge wa jimbo la Mbeya Mjini kupitia CHADEMA, Joseph Mbilinyi maarufu Sugu, na kulia ni mbunge wa sasa wa jimbo hilo, Dkt. Tulia Ackson.

Kauli hiyo ameitoa hii leo Novemba 26, 2020, wakati akizungumza na EATV&EA Radio Digital, na kuongeza kuwa hata yeye wakati anaingia kwenye hiyo ofisi zilizopo kwenye ofisi za ardhi, alikabidhiwa na halmashauri ya jiji na si yule mbunge aliyekuwepo kabla yake.

"Wewe umeshasikia wapi mbunge analia hajakabidhiwa ofisi, hakuna kitu kama hicho, aliyempa cheti cha ubunge ndiye angemwelekeza kwamba kinachofuata ni nini, afanye kazi aachane na Sugu", amesema Sugu.

Aidha Sugu ameongeza kuwa, "Yeye afuate utaratibu pengine hata sasa wamempa ofisi nyingine yeye ni mtu wa kujimwambafai, labda ofisi niliyokuwa naitumia mimi ni ndogo nadhani haitaki anatafuta 'justification' wampe ofisi kubwa zaidi kwa kusema Sugu hajanikabidhi ofisi, ofisi ni mali ya jiji".

Jumatatu ya Novemba 23, 2020, mbunge wa jimbo hilo Dkt. Tulia Ackson, wakati akizungumza na wanahabari nyumbani kwake, jijini Mbeya, alisema kuwa bado hajakabidhiwa ofisi aliyokuwa akiitumia mbunge Sugu na kwamba ataendelea na majukumu yake hawezi kumngoja kwani mlolongo ni mrefu.