Ijumaa , 28th Apr , 2023

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa Jeshi la Polisi nchini kujitathmini mara kwa mara ili kuwa tayari kukabiliana na changamoto za nyakati hizi za mabadiliko makubwa kiteknolojia na kiuchumi.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa ufunguzi wa Mradi wa kituo cha Polisi Daraja “A” Gezaulole – Kigamboni mkoani Dar es salaam uliogharimu shilingi milioni 899. Amesema Jeshi la Polisi linatakiwa kuwa kioo cha jamii katika usimamizi wa sheria hivyo ni vema kusimamia maadili mema, nidhamu kazini na uwajibikaji kwa wananchi.

Aidha Makamu wa Rais ameliasa Jeshi la Polisi kuongeza jitihada katika kukabiliana na ajali za barabarani hapa nchini, na kusema ni vyema pia Jeshi la Polisi likaangalia uwezekano wa kutumia TEHAMA na kuweka adhabu kali kwa wanaosababisha ajali pamoja na kuacha kupokea rushwa kutoka kwa madereva na kufumbia macho makosa ambayo kugharimu maisha ya watu wengi. Makamu wa Rais amesema bado taifa linakabiliwa na changamoto ya ajali ambazo zinasababishwa na madereva kutozingatia sheria za usalama barabarani, ulevi, ubovu wa magari pamoja na wengi wao kutokuwa na sifa za udereva.

Pia Makamu wa Rais ametoa wito wa kuimarishwa mahusiano baina ya Jeshi la Polisi na Wananchi ili kudhibiti uhalifu kwa urahisi, huku akieleza Uhusiano mzuri kati ya Jeshi la Polisi na raia utawawezesha wananchi kushirikiana na Polisi kudhibiti uhalifu na pia kuboresha ulinzi shirikishi hivyo ni muhimu kwa Jeshi hilo kuandaa mazingira salama ambayo yatawafanya wananchi kuwa na imani kwamba watasikilizwa, hawatadhalilishwa au kuchukuliwa kama wahalifu.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhandisi Hamad Masauni amesema Jeshi la Polisi halitashindwa kuthibiti uhalifu wowote ikiwemo uvunjifu wa maadili unaojitokeza hivi sasa. Uzinduzi wa Vituo hivyo ni katika kuadhimisha miaka 59 ya Muungano ambao una lengo la kuimarisha udugu na usalama na hivyo kuwafanya wananchi kufanya shughuli za kiuchumi kwa amani na utulivu.