Jumamosi , 11th Aug , 2018

Jeshi la polisi mkoani Mtwara limewaonya wanasiasa wanaofanya mikusanyiko isiyo halali kwa madai ya kulinda kura katika uchaguzi mdogo unaotegemewa kufanyika kesho Jumapili huku lilikitoa wito kwa wananchi kujitokeza kutekeleza haki yao ya kidemokrasia na kumchagua kiongozi wanayemtaka.

Kamanda wa polisi mkoa wa Mtwara, Lucas Mkondya.

Akizungumza leo Agosti 8 Kamanda wa polisi mkoa wa Mtwara, Lucas Mkondya amesema jeshi hilo limejipanga na lina askari wa kutosha kutuliza ghasia katika Uchaguzi wa madiwani na ubunge kesho .

Tutatakuwa na askari wengi sana katika vituo vyote vinavyotarajiwa kupigwa kura, kwa hiyo mtu yeyote asijipe jukumu hilo, hivyo vyama vinavyojipanga kutekeleza jukumu la polisi hatujaomba msaada sisi,” amesema

Kwa upande wao tume ya taifa ya uchaguzi(NEC), imeridhia kufanyika kwa uchaguzi mdogo wa Ubunge jimbo la Buyungu na madiwani Tanzania bara baada ya kuridhika na uendeshaji wa kampeni kwa vyama mbalimbali ambazo zinamalizika rasmi hii leo.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa tume ya taifa ya uchaguzi Jaji Semistocles Kaijage, wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu kufanyika kwa uchaguzi huo hapo kesho huku akibainisha kuwa maandalizo yote yamekamilika.

Jaji Kaijage amesema kuwa jumla ya mikoa 19 na halmashauri 29 zitashiriki uchaguzi huo katika maeneo ambayo mpaka sasa hayana viongozi huku wananchi 485,203 wamejiandikisha katika maeneo hayo yanayofanya uchaguzi huku kati ya hao wapiga kura 61,680 ndio watakaopiga kura katika jimbo la Buyungu.