Alhamisi , 10th Jan , 2019

Ikiwa ni siku mbili tu tangu Rais Magufuli afanye mabadiliko kwenye Wizara ya Madini, Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Mh. Jokate Mwegelo ameuhakikishia umma wa Watanzania kuwa atapambana kwa juhudi na maarifa kuhakikisha Wanakisarawe wananufaika na Madini.

Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Mh. Jokate Mwegelo.

Mh Jokate amesema kuwa Kisarawe haiwezi kuendelea kuwa masikini na kuwa na upungufu wa huduma muhimu za Afya na Elimu wakati kuna madini katika aridhi ya kisarawe ambayo watu wa Kisarawe wamepewa zawadi na Mungu.

''Uanzishwaji wa vituo maalumu vya biashara ya madini kama ilivyoelekezwa na kuagizwa na Rais  Dr John Pombe Magufuli ni njia bora ya kuhakikisha madini yanainufaisha jamii kwa kuondoa umasikini na kuwa na jamii yenye kupata huduma bora katika nyanja zote za maisha'', amesema Jokate.

Aidha amesisitiza kuwa anaamini jambo hilo litasaidia kutimiza muono mpana na ndoto kubwa ya Rais Dr John Pombe Magufuli ya kuifanya Tanzania kuwa Taifa lenye uchumi wa kati na kuwa taifa lenye kutegemewa na mataifa mengine.

Jokate ametaja madini ambayo wilaya ya Kisarawe imejaaliwa kuwa nayo ni Madini ya udongo jasi, madini aina ya chokaa, malighafi za ujenzi kama vifusi/mchanga, mawe, na  kokoto.