Jumapili , 11th Aug , 2019

Rais Dkt John Magufuli amemtuma Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, kumwakilisha katika mazishi ya marehemu wa ajali ya moto iliyotokea mapema jana ikihusisha lori.

Kwa mujibu wa taarifa ya awali, baadhi ya mazishi yanatarajiwa kuanza leo Jumapili tarehe 11 Agosti, 2019, ambapo Rais Magufuli ameagiza katika kipindi cha maombolezo, bendera zote zitapeperushwa nusu mlingoti.

Aidha Rais Dkt. Magufuli ametangaza siku 3 za maombolezo ya kitaifa kuanzia  Agosti 10, 2019 kufuatia vifo vya watu zaidi ya 60 vilivyosababishwa na ajali ya kuungua kwa moto, wakati wakichota mafuta yaliyokuwa yakimwagika baada ya lori la mafuta kupinduka Mjini Morogoro.

Ajali hiyo imetokea jana saa 2 asubuhi ambapo lori lenye shehena ya mafuta ya petroli limepinduka jirani na Kituo Kikuu cha Mabasi cha Msamvu Mjini Morogoro wakati dereva alipokuwa akijaribu kumkwepa mwendesha pikipiki.

Pamoja na zaidi ya watu 60 kufariki dunia, watu wengine takribani 70 wamejeruhiwa na wanapatiwa matibabu katika hospitali ya Mkoa wa Morogoro na Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam.