Alhamisi , 6th Aug , 2020

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli, amewashukuru wapinzani kwa kuanza kumpigia kampeni mapema, kwa kuwa wengi wao wameanza kumpa kauli za kwamba atapigiwa kura na vituo vya afya, kwa kuwa hao wanaovitumia ndiyo watakaompa kura.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli.

Kauli hiyo ameitoa hii leo Agosti 6, 2020, kwenye Ofisi Kuu za chama hicho zilizopo Dodoma, mara baada ya kuwasili katika ofisi hizo akitokea kwenye ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi alikoenda kuchukua fomu ya kuwania Urais kwa muhula wa pili

“Mtu akisema nitapigiwa kura na vituo vya afya, najua ndio wameshaanza kunipigia kampeni wao na ninawashukuru sana wanaosema hivyo, maana vituo vya afya wametibiwa wanawake watanipigia kura, Wazee hata walevi walilala humo watanipigia na inanipa nguvu kwamba ushindi wa mwaka huu utakuwa mkubwa" amesema Rais Magufuli.

Aidha Rais Magufuli akazungumza namna ambavyo, kampeni zitafanyika kwa mwaka huu, "Tulimtanguliza Mungu wakati wa Corona tukafunga siku 3, tukamshukuru siku 3 leo hakuna mwenye Corona hapa tunabanana tu hata Kitandani bananeni tu vizuri, ninasema hivyo kwa sababu aliyenitangulia amesema kampeni tutafanya Kitanda kwa Kitanda".