Jumatatu , 12th Feb , 2024

Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Dkt Jakaya Mrisho Kikwete, amesema alipokea kwa mshituko mkubwa taarifa za kifo cha Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowassa, aliyefariki wakati akipatiwa matibabu JKCI kutokana na maradhi ya kujikunja utumbo, mapafu na shinikizo la damu.

Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Dkt Jakaya Mrisho Kikwete

Dkt Kikwete ametoa kauli hiyo leo Februari 12, 2024, mara baada ya kufika nyumbani kwa Lowassa Masaki Dar es Salaam kwa ajili ya kutoa pole.

"Nimepokea kwa mshituko taarifa ya kifo nilikuwa nafahamu kwamba anaumwa lakini sikutegemea kwamba ingefikia hapa ilipofikia, ninamfahamu marehemu kwa muda mrefu tulikuwa vijana pamoja, tulikuwa chuo kikuu pamoja, tukatangulia sisi kuingia kwenye chama na yeye akafuata na tumefanya kazi pamoja kwenye chama kwa muda huo wote," amesema Kikwete

Aidha Kikwete ameizungumzia safari yao ya kugombea urais iliposhindikana mwaka 1995 lakini baadaye 2005 ikaja kufanikiwa kwake, "2005 tukajiandaa na mimi nikapata nafasi ya kuchaguliwa kuwa Rais mwenzangu akaja kuwa Waziri Mkuu tukapata changamoto katikati mwenzangu ikabidi akae pembeni, tumeendelea kuwa marafiki tukishirikiana kwa kila linalowezekana, ameugua Mwenyezi Mungu amechukua roho yake, ninachoshauri tu tuendelee kumuombea, Mungu aipokee roho yake aiweke mahali pema peponi, Edward ametoa mhango mkubwa katika Taifa letu, yaliyotokea ni changamoto katika maisha lakini hayafuti yale mema na mazuri aliyolifanyia Taifa letu,".

Edward Lowassa atazikwa Februari 17 mwaka huu wilayani Monduli mkoani Arusha, shughuli ya mazishi itaongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.