Kauli ya Nassari baada ya kuvuliwa Ubunge

Ijumaa , 15th Mar , 2019

Aliyekuwa mbunge wa Arumeru Mashariki (CHADEMA), Joshua Nassari amedai kuwa kitendo cha kuvuliwa ubunge ni uonevu dhidi yake, na kusisitiza kuwa fikra hizo zipuuzwe.

Joshua Nassari.

Nassari ametoa kauli hiyo ikiwa ni siku moja tangu Spika Ndugai alipomwandikia barua Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC,) Jaji Semistocles Kaijage kumtaarifu kuhusu jimbo hilo la Arumeru Mashariki kuwa wazi baada ya mbunge wake kupoteza sifa.

Nassari amesema kuwa kesho atazungumza na vyombo vya habari kwa undani, na kuahidi kuitafuta haki popote na kwamba alikuwa kimya kwa kuiheshimu sheria.

"Watanzania wenzangu na Watu wangu wa Meru. Tumefanyiwa dhuluma na uonevu. Nitazungumza kesho na vyombo vya habari kwa undani kuhusu jambo hili. Tutaitafuta haki popote.  Katika hatua ya sasa, puuzeni fikra hasi zinazoenezwa na maadui zetu dhidi yangu, hata hivyo niliheshimu sheria na vielelezo vipo", ameandika Nassari.

Mbunge huyo amevulia ubunge akiwa anatekeleza majukumu ya kibunge kwasababu alikuwa katika ziara ya kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii iliyokuwa Chuo cha Mwika, Moshi mkoani Kilimanjaro.