Kilichojiri kesi ya 'Boss' aliyemuua dada wa kazi

Alhamisi , 26th Mar , 2020

Mtuhumiwa wa kesi ya mauaji ya mfanyakazi wake wa ndani aitwaye Salome Zakaria, Mkami Shirima mwenye umri wa miaka (30), leo Machi 26, 2020, amefikishwa tena kwa mara ya pili katika Mahakama ya Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha kwa ajili ya kesi yake kutajwa.

Mkami Shirima, alivyofikishwa mahakamani leo.

Imeelezwa kuwa mwanamke huyo alifikishwa mahakamani hapo majira ya saa 3:00 asubuhi, akiwa amejifunika sura yake kwa kipande chekundu cha khanga, katika kesi yake namba 5 ya mwaka 2020.

Akizungumza mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo Amalia Mushi, Wakili wa Serikali Abelaide Kasala, amesema kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa, ambapo kesi hiyo imeahirishwa hadi Aprili 8, 2020, itakapotajwa tena.

Mkami Shirima anadaiwa kutenda kosa hilo, baada ya kumpiga hali inayodaiwa kupelekea kifo cha mfanyakazi wake huyo wa ndani, mnamo Machi 5, 2020, baada ya kumtuhumu amemuibia elfu hamsini (50,000).