Alhamisi , 28th Mei , 2020

Mtanzania anayeishi nchini Marekani Fanirani Mbasha, amesema kuwa mpaka sasa hivi wale Askari wanne waliokuwepo katika tukio la mtu mweusi nchini humo aliyekandamizwa kwa goti shingoni mwake na kupoteza maisha wamekwishafukuzwa kazi.

Upande wa kushoto, Askari akionekana kumkandamiza raia mweusi, kulia ni Mtanzania anayeishi nchini Marekani Fanirani Mbasha.

Fanirani ameyabainisha hayo leo Mei 28, 2020, wakati akizungumza na kipindi cha SupaBreakfast ya East Africa Radio, na kusema kuwa mpaka sasa hivi raia weusi nchini Marekani bado wako nje wakiandamana, kudai hatua kali zaidi zichukuliwe dhidi ya Askari hao ikiwemo kupewa mashtaka ya mauaji.

"Nadhani presha hii inaweza ikazaa matunda kwa sababu mpaka sasa hivi bado waandamaji wako nje, ukiangalia kwenye live stream unaona kabisa hawa watu hasira zao bado hazijaisha, licha ya kwamba hao Askari wamefukuzwa kazi na watu wanatamani hatua kali zaidi zichukuliwe na wapewe mashtaka" amesema Fanirani.

Hivi karibuni kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii, zilisambaa video zikionesha Askari akiwa amemkandamiza kwa kutumia goti lake shingoni raia mweusi, huku mtu huyo akionekana kulalamika na bila kusikilizwa na ndipo mauti yalimpofika, na watu wengi wamelaani kitendo hicho.