
Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un amesema yuko tayari kuanza tena mazungumzo na Marekani iwapo Washington haitaiambia Pyongyang kuachana na mpango wake wa silaha za nyuklia, vyombo vya habari vya serikali ya Korea Kaskazini vimeripoti jana Jumatatu, Septemba 22, 2025.
Kulingana na Shirika la Habari la Korea Kaskazini (KCNA), Kim Jong Un amesema, "Ikiwa Marekani itaachana na tamaa yake ya upotoshaji ya kutaka tusitishe shughuli zetu za nyuklia na, kwa kutambua ukweli, inataka kweli kuishi pamoja nasi kwa amani, basi hakuna sababu kwa nini hatuwezi kuketi na nchi hiyo kwenye meza ya mazungumzo".
Kati ya mwaka 2006 na 2017 Korea Kaskazini ilifanya majaribio sita ya nyuklia na tangu wakati huo imeendelea kutengeneza silaha zake licha ya vikwazo vikali vya kimataifa.
Pyongyang inahalalisha mpango wake wa kijeshi wa nyuklia ili kukabiliana na vitisho kutoka kwa Marekani na washirika wake, ikiwemo Korea Kusini. Mnamo mwezi Januari, Kim Jong-un alisema kuwa programu hii itaendelea kwa muda usiojulikana.
Akikumbukwa na wengi kwa kufanya mfululizo wa mikutano nadra na Kim Jong-un wakati wa muhula wake wa kwanza, Donald Trump ameonyesha nia tangu arejee madarakani mwezi Januari mwaka huu ili kuanza tena mawasiliano na kiongozi wa Korea Kaskazini, ambaye alimtaja kama mtu mwerevu.
Wawili hao walikutana kwa mara ya kwanza kwenye mkutano wa kihistoria mnamo mwezi Juni 2018 huko Singapore, mara ya pili huko Hanoi, Vietnam, mnamo mwezi wa Februari 2019, na mara ya mwisho kwenye mpaka kati ya Korea mbili mnamo mwezi Juni 2019. Mikutano hii haikuleta maendeleo yoyote kuhusu uwezekano wa Pyongyang kuachana na nyuklia.