Jumanne , 12th Mar , 2019

Spika wa Bunge, Job Ndugai amemkaribisha Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe pamoja na mbunge wa Tarime Ester Matiko kuendelea na shughuli za kibunge baada ya kushinda rufaa ya kupewa dhamana kutokana na kesi inayowakabili.

Mbowe akiwa na Matiko.

Baada ya kurejea uraiani, wawili hao leo Machi 12, 2019 wamekwenda bungeni kuhudhuria vikao vya kamati za Bunge ambapo Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amewasilisha mapendekezo ya Serikali ya Mpango, Kiwango cha Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2019/2020.

Kabla Waziri Mpango hajaanza kuwasilisha taarifa yake katika ukumbi wa Pius Msekwa, Spika Ndugai amesema, "Kwanza nianze kwa kumkaribisha kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni (Mbowe) na mheshimiwa Esther Matiko kwa lugha ya kibunge tunasema walikuwa Mtera".

Mbowe pamoja na Esther Matiko walikuwa mahabusu katika gereza la Segerea baada ya kufutiwa dhamana na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Hata hivyo, Machi 7, 2019 Mahakam Kuu Kanda ya Dar es Salaam iliwarejeshea dhamana yao, baada ya kushinda rufaa waliyoikata wakipinga uamuzi wa Mahakama ya Kisutu.

Bofya link hapo chini kusikiliza alichosema Spika.