
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli
Hayo yamejiri hii leo Februari Mosi, 2021, katika maadhimisho ya siku ya sheria na miaka 100 ya Mahakama, na ndipo alipowasihi Majaji na Mahakimu, kuona umuhimu wa kutumia lugha ya Kiswahili ambayo itapunguza gharama kwa Watanzania wanaotumia wakarimani kutafsiri kesi na hukumu zao.
"Nampongeza sana Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma kwa kutumia Kiswahili kutoa hukumu kwenye kesi ya North Mara Gold Mine dhidi ya Gerald Nzumbi, ninajua alisemwa sana, amekuwa mzalendo wa kwanza kwa kuandika kwa lugha ya Kiswahili na mimi leo nampandisha cheo kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa kwa uzalendo huo wa kitanzania wa kukwepa miiko iliyopo ndani ya Mahakama", amesema Rais Dkt. Magufuli.
Aidha Rais Dkt. Magufuli ameongeza kuwa, "Mimi nilipoingia madarakani niliambiwa sijui Kingereza wala sikujali kana kwamba kujua Kingereza ndiyo kusoma, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) nimekaa miaka mitatu nikisoma masomo yangu ya Sayansi, na nikakaa mwaka mzima Uingereza sijui nilikuwa nazungumza kisukuma kule, niliamua kuzungumza Kiswahili lengo ni kuki-promote".